LATEST UPDATES:

Kuomba kwa BIDII huleta matokeo makubwa | Bible & Mission Centre


Leo siku ya Ijumaa ninasikia moyoni nikushirikishe jambo kuhusu MAOMBI. Kwa kawaida ratiba nyingi za makanisa (ya ki Pentekoste) na huduma zetu, siku ya ijumaa ni siku ya maombi. Inaweza kuwa ni kufunga na kuomba...au maombi ya kukutana jioni...au maombi ya mkesha ambayo watu hukutana kanisani usiku na kuomba hadi alfajiri. Hili ni jambo jema kwa mwili wa Kristo kuwa na muda na ratiba ya kufanya maombi, na kwa sababu hii nimeona vema nikushirikishe neno la kukutia moyo na nguvu katika maombi yako leo na kila mara uombapo.
Bila shaka utabarikiwa!
Kichwa hapo juu nimesema "Kuomba kwa BIDII huleta matokeo makubwa." Huu ni ukweli usiopingika. Tusome Neno la Mungu kutoka YAKOBO 5:17 "Eliya alikuwa mwanadamu mwenye tabia moja na sisi, akaomba kwa bidii mvua isinye; na mvua haikunya juu ya nchi muda wa miaka mitatu na miezi sita."
Mfalme Ahabu aliruhusu miungu ya kigeni kuabudiwa katika taifa la Israel, ikiwa ni pamoja na BAALI (mungu wa wakanaani) aliyejulikana kuwa mwenye nguvu akiwashinda miungu wengine katika vita.
Nchi yote ilionekana kumuasi MUNGU wa kweli YEHOVA na katika maelfu ya watu wa Israel ni elfu saba tu ambao hawakuwa wamemwinamia na kumbusu Baali.....lakini hawa nao walikuwa hoi kwa woga, hata Eliya hakujua kama kuna watu kama hao, katika saa ya upweke wake.
Ili kumdhihirisha MUNGU wa kweli tena katika taifa la Israel, ilimlazimu Eliya kwenda mbali zaidi ya kawaida. Biblia inasema aliomba kwa BIDII mvua isinye (isinyeshe) kwa miaka mitatu na nusu.
Hapa kuna neno bidii.....na nilipokuwa natafakari neno hili nikagundua kuwa kuna mambo mengi tunaomba na wala hayatokei kwa sababu hatujaweka bidii katika kuyadai yatokee. Je, ni mambo mangapi umeomba na hayakutokea na mwisho wa siku ukabaki kusema "hayakuwa mapenzi ya Mungu!?" lakini ukweli inawezekana ni bidii tu ndio ilikosekana ili kupata matokeo makubwa.
BIDII ni:-
(a) Kuwa na moto, hamasa na ari....
(b) Kushikilia jambo na kukataa kubadili msimamo.
(c) Uchaji Mungu na kuwa na Imani
Kuna mambo ambayo kamwe hayataweza kutokea ikiwa hatutaomba kwa moto, hamasa na ari itokanayo na ule msukumo wa ndani (nguvu itendayo kazi ndani yetu). Na kuna mambo ambayo tunatakiwa kushikilia kwa nguvu na kukataa kubadili msimamo hata kama tunaona haiwezekani.
Imani yetu kwa Mungu tunayemuomba na uchaji wetu vitatuletea matokeo makubwa tunapoomba.
☆ Eliya aliweza kusimamisha mvua ili taifa la Israel limrudie Mungu YAHWEH alipoomba kwa BIDII.
☆ Uamsho uliotokea Korea Kusini katika kanisa la YOIDO SUNBOGEUM CHURCH miaka ya 70 ulitokea kwa sababu waliomba kwa BIDII.
☆ Uamsho uliotokea Pensacola Florida-Marekani miaka ya 90 ni kwa sababu waliomba kwa BIDII.
1 Thes 5:17 "Ombeni bila kukoma" kwa maneno mengine ni sawa na kusema ombeni kwa bidii!
Ni wito wangu kuwa utadumu katika maombi mpaka upate matokeo makubwa ya kile unachoomba kwa Mungu akutendee.
Tusipoomba kwa bidii maana yake sisi tulioitwa kwa jina la BWANA tunapaswa kulaumiwa kwa kila uovu na ubaya unaotokea katikati yetu.
Bwana ataiponyaje nchi ikiwa walioitwa kwa jina lake hawaombi kwa bidii?
Kuna neno hili PUSH ambalo watu wamesema ni "Pray Until Something Happens" nami nasema endelea ku-push mpaka uone matokeo mtu wa Mungu.
Mungu akubariki sana.

1 comment:

  1. Be blessed my pastor, I have been following your teachings, since you started to teach, real it has been a way of growing high faithly everyday to me, keep on My pastor my brother my Role model......your blessed I will in Arusha at the end of this week, I will try to fix my schedule in order to join you next Sunday be blessed once again

    ReplyDelete