LATEST UPDATES:

Kwanini tunamuabudu Mungu? | Bible & Mission Centre

Kwanini Tunaabudu?

Ni nini maana ya Kuabudu?
Ni tendo linalogusa akili , hisia, nafsi na utu wa mtu na mwili pia kwa kusujudu, kuanguka kifudifudi, au uso kwa uso. Mw. 17:3 Tendo hili linafanywa pasipo ushawishi wa kitu, wala si nje ya Moyo wa kumtambua Mungu kuwa wa thamani kuliko kitu chochote anayestahili kupewa ibada ya pekee na kupelekea kujitoa kwake bila unafiki wala ubinafsi. Ni dhana zaidi ya ufahamu wetu, taratibu, desturi na mipango ya ibada, ni ibada inayojumuisha utu wako mzima na kuwasha moto katika mawazo, fikra na hisia zako zote, kiasi cha kuhisi unampapasa na kumwona Mungu katika Roho na kuwa halisi.1Yoh1.1-2,Lile lililokuako tangu mwanzo tulilolisikia ,tuliloliona na macho yetu tulilolitazama,na mikono yetu ikalipapasa kwa habari ya neno la uzima.na uzima huo ulidhihirika nasi tumeona tena twashuhudia huo uzima.Uhalisi huu unampeleka mtu kumwabudu MUNGU.

Kuabudu asili yake ni wapi?
Kuabudu asili yake ni mbinguni, kuabudu kulikuwepo kabla ya Adamu kuumbwa. Maana walikuwepo viumbe kabla ya Adamu huko mbinguni waliomwabudu Mungu. Ibada ina asili katika Mungu mwenyewe, Uungu una asili ya kuabudiwa kwa hiyo chanzo cha ibada ni Mungu. Ayubu 38:4-7, Zaburi 148:2-14. Hapa tunaona malaika wanamwabudu na kumsifu Mungu. Mstari wa 5 zaburi 148 unaonyesha agizo la Mungu akiagiza viumbe vyote kumwabudu na kumsifu kutoka mbinguni mpaka duniani kuanzia viumbe vyenye uhai na visivyo na uhai

Kwanini Bible & Mission Centre tumejikita kwenye kuabudu?

Wakati wa kuabudu ni wakati muhimu mno, ni wakati wa shughuli ya utukufu kupita zote ambazo mwanadamu anafanya katika maisha yake, wakati wa kuabudu unazidi nyakati zote anazoweza kuzifurahia, tena kuabudu huacha kumbukumbu ndani yake, kumbukumbu ya kuabudu inapita vilele vyote vya furaha hizo maana ni wakati wa kukutana na Mungu. Je mwanadamu ninani hata akapewa nafasi tukufu kama hiyo? Kwakuwa, kuabudu ni sehemu ya maisha na ushirika na Mungu na ni jambo la rohoni, basi, kuabudu kunakuwa sehemu ya kila jambo tunalolifanya, na ni ufunguo wa maisha yenye mafanikio na mwelekeo wa fikra na mawazo ya moyo, na kuwa mtindo wa maisha maana Kuabudu kunahusisha hisia kali zenye upendo mkuu zinazogusa ufahamu na kuzama katika upendo wa ndani kabisa na kuhusudu. (Adoration) Kuhusudu ni mguso ambao unaachilia hisia za papo kwa hapo, na kusema kwa sauti ya kusikika maneno yenye kujaa mlipuko wa upendo mkuu, na kwa sauti ya upole na kugugumiza maneno, pamoja na ubembelezi mwingi, ukiambatana na maombi yaliyojaa unyenyekevu, heshima , adabu, na hofu na kijikita katika ibada ya dhati mbele ya Mungu, kumsifu na kumwabudu. 

Somo litaendelea Jumanne ijayo, Subscribe ili uwe wakwanza kupokea updates mara tu tunapochapisha chapisho lolote.
MUNGU AKUBARIKI WEWE UNAESOMA UJUMBE HUU
Karibu BIBLE & MISSION CENTRE

No comments